Leviticus 8:14-24

14 aKisha akamtoa fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi, nao Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 15 bMose akamchinja yule fahali na akachukua sehemu ya hiyo damu, kisha kwa kidole chake akaitia kwenye pembe zote za madhabahu ili kutakasa madhabahu. Akaimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Kwa hiyo akayaweka wakfu ili kufanya upatanisho kwa ajili ya madhabahu. 16 cPia Mose akachukua mafuta yote yanayozunguka sehemu za ndani, mafuta yanayofunika ini, figo zote mbili pamoja na mafuta yake, akayateketeza juu ya madhabahu. 17Lakini fahali, ikiwa pamoja na ngozi yake na nyama yake na sehemu zake za ndani na matumbo, akaiteketeza nje ya kambi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

18 dKisha Mose akamleta kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 19Ndipo Mose akamchinja yule kondoo dume na kunyunyiza damu yake pande zote za madhabahu. 20Mose akamkata yule kondoo dume vipande vipande na kukiteketeza kichwa, vile vipande na yale mafuta. 21Kisha akamsafisha sehemu za ndani na miguu kwa maji, na kumteketeza yule kondoo dume mzima juu ya madhabahu kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kupendeza, sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa moto, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

22Kisha akaleta kondoo dume mwingine, ndiye kondoo dume kwa ajili ya kuwaweka wakfu, naye Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake. 23 eMose akamchinja yule kondoo dume, akaichukua sehemu ya damu yake na kuipaka juu ya ncha ya sikio la kuume la Aroni, na juu ya kidole gumba cha mkono wake wa kuume na juu ya kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 24 fPia Mose akawaleta hao wana wa Aroni mbele, akaipaka sehemu ya hiyo damu kwenye ncha za masikio yao ya kuume, juu ya vidole gumba vya mikono yao ya kuume, na juu ya vidole vikubwa vya miguu yao ya kuume. Kisha akanyunyiza damu pande zote za madhabahu.
Copyright information for SwhNEN